YOUR MOST FAVORITE BLOG.

YOUR MOST FAVORITE  BLOG.
Calvin

Wednesday 3 July 2013

OBAMA AWAOMBA RADHI WATANZANIA: SOMA HAPA


Kana kwamba alisikia kilio cha wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa na shauku ya kumwona lakini ikashindikana, Rais Barack Obama wa Marekani amewaomba radhi kwa hali hiyo.
Akizungumza juzi wakati wa dhifa iliyoandaliwa kwa ajili yake na ujumbe wake na Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Dar es Salaam, Obama alisema akirudi nchini siku zijazo, atapita mitaani akiwa katika gari la wazi.
CONTINUE READING

"Niliona wananchi walivyojitokeza kwa wingi kutupokea barabarani, nilifarijika sana lakini hawakuweza kutuona vizuri kwani tulikuwa ndani ya gari maalumu-The Beast.

"Miaka ya sitini Rais John Kennedy alipokuja hapa, alipita na gari la wazi mitaani wananchi wakamwona, naomba radhi nikija tena nitaonekana," alisema Obama. 

Watu wengi waliozungumza na vyombo vya habari walionesha dhahiri kiu ya kutaka kumwona Rais huyo wa kwanza mweusi wa Marekani, lakini wakaishia kuona gari lake ambalo hata hivyo, lilipita kwa kasi barabarani kwenda Ikulu na kurudi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Kama ilivyokuwa imezoeleka huko nyuma, Rais wa nchi ambaye amekuwa akifika nchini kwa mara ya kwanza, amekuwa akipita mitaani kwa gari la wazi sambamba na mwenyeji wake akisalimiana na wananchi, hiyo imekuwa ikifanyika pia kwa wasanii wa kigeni.

Hata hivyo, safari hii ulinzi ulionekana kuwa mkali katika ujio wa Rais Obama na kusababisha wenye kiu ya kumwona moja kwa moja kushindwa kufanya hivyo isipokuwa waliokuwa na uwezo wa kufika uwanjani na katika shughuli alizofanya maeneo kadhaa jijini.

Mapema, Rais Kikwete alimhakikishia Rais Obama kwamba kuanzia sasa Afrika itapenda kuona ongezeko la uwekezaji na uhusiano wa kibiashara baina yake na Marekani.

Kikwete alisema hayo juzi usiku katika Ikulu ya Dar es Salaam katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia Rais Obama ambaye alimalizia ziara yake jana.


"Hii inaweza kuwa katika ngazi ya mataifa mawili au Taifa la Marekani na eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki,"alisema Kikwete.

Alimwambia uzinduzi wa Mpango wa Nishati ya Umeme kwa Afrika wenye lengo la kusaidia nchi za Kiafrika kukabiliana na upungufu wa nishati hiyo ni msaada ambao umekuja kwa wakati mwafaka.

Alisema Afrika imekuwa ikilenga kuwa na uchumi mkubwa na hatimaye kujiletea maendeleo, lakini kikwazo kikubwa kimekuwa ni tatizo la umeme wa kutosha.

"Hatua hii ya Marekani kusaidia katika eneo hilo, itakwenda sambamba na kuwezesha mataifa ya Afrika kuibua uwezo wao wa kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watu wao," alisisitiza Kikwete.

Alisema hatua hiyo itaimarisha ushindani, itakuza maendeleo ya viwanda na kufanya nchi za Afrika kushiriki vizuri katika uchumi wa dunia na kuwa wabia katika biashara ya kimataifa badala ya kuwa wapokeaji wa misaada ya kigeni.

"Tunakupongeza kwa uongozi wako katika kukabiliana na changamoto za maendeleo na usalama zinazolikabili bara la Afrika. Umekuwa kishawishi kikubwa kwetu, tunaoamini katika demokrasia, uhuru wa mtu, fursa sawa, kutokuwa na ubaguzi na kuwa na Afrika isiyo na migogoro.

"Wewe ni rafiki wa kweli wa Tanzania na Afrika, siku zote tutaenzi amali hizo katika nyoyo na fikra zetu,"Kikwete alimwambia Obama.

Alieleza matumaini ya Watanzania kwamba Obama atapata fursa nyingine ya kuja nchini na kukaa angalau kwa muda mrefu kidogo ili ajionee mengi nchini; nchi ambayo ina vivutio kama Mlima Kilimanjaro, hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na kisiwa cha marashi cha Zanzibar. 

Rais Kikwete alimshukuru Rais Obama na Serikali yake na watu wa Marekani kwa msaada wao endelevu kwa Serikali na watu wa Tanzania.

"Msaada wenu katika chakula, elimu, afya, barabara, umeme na maji umesaidia kuboresha maisha ya watu wengi nchini Tanzania.

"Naamini uendelevu wa msaada huo utamaanisha watu wengi kuondokana na umasikini. Kauli yako ya kutuhakikisha kwamba Serikali yako itaendelea kuisaidia Tanzania katika maendeleo imepokewa nasi kwa mikono miwili na unyenyekevu mkubwa," alisema Kikwete.

Akiwa Symbion, Rais Obama aliihimiza Serikali kuhakikisha miradi ambayo itaanzishwa chini ya mpango wa Power Africa utekelezaji wake uharakishwe ili kutoa fursa kwa wananchi kuona manufaa yao katika kujipunguzia umasikini.

Alisema katika mpango huo ambao Serikali yake imeahidi kutoa dola za Marekani bilioni 7, alisema sekta binafsi ambayo itahusishwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wake itatoa dola za Marekani bilioni 9.

Alisema kutakuwa na manufaa makubwa iwapo mpango huo utahusisha Serikali na sekta binafsi kwa upande mwingine akiongeza kuwa dhamira ya sekta binafsi katika kutoa kiasi hicho cha fedha inaonesha nia ya Marekani kuinua Afrika yenye nuru," alisema Rais Obama akionesha matumaini ya mpango huo ambavyo unaweza kunufaisha nchi nyingi za Afrika. 

Obama ambaye aliitumia hotuba hiyo kuaga Watanzania, alisema Symbion ni mfano wa miradi ambayo Marekani imedhamiria kuitekeleza Afrika ya kuongeza maradufu uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo lengo ni kupunguza umasikini katika bara hilo. 

Alisema ili miradi hiyo iwe na manufaa kwa nchi husika kote alikopita, alitoa mwito kwa viongozi kuhakikisha utekelezaji unaharakishwa ili kunufaisha nchi na kwa watu. 

Alikemea tabia ya ucheleweshaji wa miradi katika Afrika ikiwamo ya umeme lakini akasema ana imani na uongozi wa Rais Kikwete kuwa mpango huo utatekelezwa kwa kasi. "Ni lazima tuongoze katika utekelezaji wa miradi hii na naamini chini ya Rais Kikwete hili linawezekana."

Alisema ili kufanikisha kuwa na umeme wa uhakika ni vema kupunguza urasimu katika kuhudumia wawekezaji wa sekta ya umeme ili wapate nafasi ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi.

Aliongeza kuwa ufanikishaji wa mpango huo utakuwa ni hatua ya ushindi kwa pande zote; yaani kwa Tanzania ambayo itapata umeme wa uhakika ambao utasaidia kupunguza umasikini, lakini pia kwa Marekani ambako wafanyabiashara watapata fursa ya kuwekeza nchini.

Pia alitaka sheria na taratibu zifuatwe na kuheshimiwa katika masuala yote ya uwekezaji ambao utahusisha miradi itakayoanzishwa chini ya mpango wa Power Africa.


Alipoingia ndani ya mitambo ya Symbion, Rais Obama alikabidhiwa mpira wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa gesi.

Mpira huo ambao umebuniwa na vijana wa Kimarekani, unafaa kwa matumizi vijijini kwani unaweza hata kuchaji vifaa vya umeme kama simu ambapo pia gesi hiyo ina uwezo wa kuwasha taa inayoweza kutumika kumulika ndani ya nyumba.

Rais Obama alizindua mipira hiyo ambayo itapatikana hivi karibuni nchini kwa kumpasia Rais Kikwete na kueleza matumaini yake kuwa inaweza kuwa na manufaa makubwa katika maeneo ambako hayajafikiwa na umeme.

Kampuni ya Symbion yenye makao yake makuu Washington, Marekani imeajiri Watanzania 1,000 na Rais Obama jana alitangaza kuwa ni kampuni pekee ambayo itasimamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme inayofadhiliwa na Serikali ya watu wa Marekani.

Symbion kwa sasa inatekeleza miradi yenye uwezo wa kuzalisha umeme katika nchi za Afrika Mashariki na Magharibi ambayo imepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Katika miaka mitano, kampuni hiyo imepanga kuwekeza kiasi cha Sh trilioni 3 katika uzalishaji umeme na njia za kuusafirisha.

Kati ya miradi hiyo, umo wa gesi unaojengwa Mtwara wenye uwezo wa megawati 400 na unaendeshwa kwa kushirikiana na kampuni nyingine ya Marekani ya General Electric (GE) itakayotoa vifaa vya ujenzi katika mradi huo ambao unahusisha ujenzi wa njia ya umeme yenye umbali wa kilometa 650.

Nchini, kampuni hiyo kwa sasa inamiliki vituo vitatu vya kuzalishia umeme wa jumla ya megawati 217 ambavyo vipo Dar es Salaam, Dodoma na Arusha. Kituo cha Ubungo cha Symbion kinazalisha megawati 112 kwa gesi na ndiyo kampuni inayozalisha umeme mwingi unaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Mitambo hiyo imetengenezwa mjini Houston, Texas na inaelezwa kuwa ya kisasa zaidi yenye uwezo mkubwa wa kufua umeme kwa kasi kama ilivyo injini ya ndege. Mitambo hiyo awali ilikuwa ya Dowans ambayo iliileta nchini baada ya kupewa zabuni ya kufanya hivyo na Kampuni ya Richmond.

Awali baadhi ya wabunge walishauri inunuliwe na Serikali, lakini baadhi yao walikataa kuwa ni mitumba na sheria ya manunuzi hairuhusu. Lakini mitambo hiyo ambayo baadhi ya Watanzania waliikejeli leo ndiyo kimbilio la Serikali kutokana na vyanzo vya kufua umeme wa maji kupungua uwezo wake.


Kutokana na mapenzi mengi waliyonayo Watanzania kwa Obama, jana maelfu ya watu walikusanyikwa Ubungo ili kumwona Rais huyo mweusi wa Marekani.

Tangu saa mbili asubuhi Ubungo ilishafurika watu na hadi anawasili eneo hilo saa 5 asubuhi umati huo ulishaongezeka hali inayoonesha kuwa Rais huyo ni kipenzi cha Watanzania.


Baada ya kukagua mitambo ya Symbion, Rais Obama alisindikizwa na mwenyeji wake, Rais Kikwete hadi uwanja wa ndege na akapanda ndege yake ya Air Force One na kurejea Marekani.

No comments:

Post a Comment

gfjythfghgfhdfgergdfgbvdfgrfdgdfrgdrgdfrgrdegedrgdrfg