YOUR MOST FAVORITE BLOG.

YOUR MOST FAVORITE  BLOG.
Calvin

Thursday 20 November 2014

HIVI NDIVYO MWAKYEMBE ALIVYOSULUBIWA


Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana ilimsulubu Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ikieleza kuwa wizara yake iliingia mkataba wa mradi wa treni za kisasa kutoka Stesheni ya Dar es Salaam hadi Pugu kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) bila kufuata taratibu.
Kambi hiyo ililieleza Bunge kuwa mkataba huo ulisainiwa baina ya mmiliki wa Kampuni ya M/s Shumoja, Robert Shumake na Shirika la Reli Tanzania huku Waziri Mwakyembe akishuhudia.
Msemaji Mkuu wa kambi hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Uwekezaji na Uwezeshaji, Pauline Gekul alitoa madai hayo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).
Gekul alisema taratibu hazikufuatwa kwa kuwa haieleweki ni lini Serikali, wakala au Wizara ya Uchukuzi ilitangaza zabuni ya mradi wa treni kutoka Stesheni hadi Pugu kupitia JNIA.
“Pia haijulikani ni lini Serikali ilifanya upembuzi yakinifu kuhusu mradi huo wa reli kwa kufuata taratibu kama zinavyoainishwa na Sheria ya PPP ya mwaka 2010 ambayo inafanyiwa marekebisho hivi sasa,” alisema Gekul na kuongeza: “Haijulikani ni kampuni ngapi ambazo ziliomba tenda ya ukandarasi wa treni na kwamba M/s Shumoja ilishinda tenda hiyo kwa vigezo gani.”
Alisema kwa kifupi ni wazi kuwa Dk Mwakyembe na wizara yake walikiuka vifungu vya Sheria ya PPP. Alivitaja vifungu hivyo kuwa ni 4(1) na (2) vinavyomtaka waziri kutangaza katika Gazeti la Serikali miradi mbalimbali inayotegemewa kufanywa na sekta ya umma kwa ubia na sekta binafsi.
Gekul alisema pia kifungu cha 5(1) kilikiukwa ambacho kinaitaka mamlaka inayohusika kufanya upembuzi yakinifu baada ya kupembua mradi ambao utafanywa kwa ubia.
“Pia kifungu cha 9 kinachotaka mzabuni kutoa nyaraka mbalimbali za miradi ikiwamo jina, mahesabu yaliyofanyiwa ukaguzi pamoja na vielelezo vya uwezo wa kifedha,” alisema Gekul.
Alihoji kulikuwa na uharaka gani wa utekelezaji wa mradi huo ambao umekiuka Sheria ya PPP bila kuwahusisha wadau wengine ambao wangeweza pia kushindana na Shumoja?
“Ingekuwa ni vyema kama Serikali ingeweka bayana undani wa mkataba wa mradi huo ambao kama Watanzania hatujawahi kusikia ukitangazwa ili kutoa fursa kwa wazabuni wenye uwezo kushindania zabuni hiyo zaidi ya kuona na kuusikia mradi siku ya utiaji saini,” alisema.
Alisema Serikali ikishabanwa kutoa majibu juu ya uvunjwaji wa sheria, huja na majibu ya kejeli, hivyo Watanzania waelewe kuwa sheria zimekuwa zikipindishwa ili kupitisha miradi ambayo baadaye hugeuka kuwa mzigo kwao kama ilivyokuwa IPTL na Escrow.
Alisema pamoja na adha ya usafiri jijini Dar es Salaam, ukweli utabaki palepale kwamba, Dk Mwakyembe alisimamia mchakato wa mradi uliokiuka sheria ambao ikiwa utashindikana katika utekelezaji na mzigo wa uvunjwaji ama usitishwaji wa mkataba, gharama zitarudi kwa Watanzania.MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

gfjythfghgfhdfgergdfgbvdfgrfdgdfrgdrgdfrgrdegedrgdrfg