YOUR MOST FAVORITE BLOG.

YOUR MOST FAVORITE  BLOG.
Calvin

Tuesday 2 September 2014

WARAKA WA MAKANISA KUHUSU KATIBA MPYA WAZAGAA MITAANI




Iringa. Waraka uliotolewa juzi na Jukwaa la Wakristo Tanzania wakitaka mchakato wa Katiba Mpya usitishwe, jana ulisomwa katika baadhi ya makanisa na sasa utasambazwa katika jumuiya ndogo za Kanisa Katoliki.
Akizungumzia waraka huo katika Ibada ya Jumapili, Paroko wa Parokia ya Mkwawa ya Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa, Padri Oscar Rutechura alisema amechukua uamuzi huo ili kuwawezesha waumini kuelewa vizuri tamko la viongozi wao wa dini kuhusu mchakato wa katiba unaoendelea.
“Katika ibada hii ya leo nitatoa mahubiri kwa muda mfupi, nitafanya hivyo ili niweze kufanya mambo mengi yaliyoko mbele yangu,” alisema Padri Rutechura kabla ya kusoma waraka huo.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).
Padri Rutechura alitaja mapendekezo sita yaliyomo kwenye waraka huo ambayo ni: Kuitaka Serikali irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kulitaka Bunge kuboresha maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba na kuacha kuyadharau na kuyapuuza.
Mengine ni kutaka mchakato wa Katiba usitishwe, Bunge la Katiba liendeshwe kwa mujibu wa kanuni, wananchi waendelee kusoma na kufuatilia mchakato na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihusishwe na kupewa mamlaka ya kujibu maswali yanayojitokeza.
Padri Rutechura alisisitiza kuwa ametumiwa waraka huo na Askofu wa Jimbo la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye kwa sasa ndiye Rais TEC kwa ajili ya kuusoma kwa waumini wote.
Alisema baada ya kuusoma angetoa nakala na kuzigawa kwa viongozi wa jumuiya ndogondogo ili waumini wote wa parokia hiyo wapate fursa ya kuusoma na kuuelewa na watoe uamuzi sahihi.
Padri Rutechura aliwataka waumini kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu la wapigakura pindi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itakapotangaza kuanza kuandikisha upya wapigakura.
Alisema hatua hiyo itawasaidia waumini hao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupiga kura ya maoni kupata Katiba Mpya au kuipinga, kuchagua viongozi wanaofaa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Wakati huohuo, polisi wilaya mpya ya kipolisi, Mbalizi mkoani Mbeya wamewakamata waumini 16 wa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Songwe kwa madai ya kutaka kufanya vurugu kwenye kanisa lao.
Paroko wa Parokia hiyo, Ernest Mwashiuya alisema waumini hao walikamatwa jana na kwamba taarifa zaidi zitatolewa na polisi.
Baadhi ya waliokamatwa walisema tukio hilo lilitokea Jumamosi saa 12 jioni wakati wanajadili sehemu ya kusalia ibada ya Jumapili baada ya kutokuwa na imani na paroko wao. Walisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Paroko Mwashiuya, Jumapili ya Agosti 24 kutamka kwamba waumini wasio na imani naye wasifike kanisani hapo tena.
“Polisi walifika nyumbani kwa Emmanuel Kalomba tulikokuwa tukisali na kutukamata,” alisema mmoja wa waumini waliokamatwa na kuachiwa kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment

gfjythfghgfhdfgergdfgbvdfgrfdgdfrgdrgdfrgrdegedrgdrfg