wabaini kuondolewa kipengele cha mkataba
- SUNDAY, 20 JANUARY 2013
- Imeandikwa Na: Mjengwa Blog
MAWAZIRI wanne wamebaini kuondolewa kipengele ndani ya mkataba kinachomtaka mkandarasi wa Kampuni ya ujenzi ya Leinton ya Singapore kuiachia Mamlaka ya Bandari (TPA) vifaa vyenye thamani ya sh bilioni 3 baada ya kumaliza ujenzi.
Mkandarasi huyo ambaye amemaliza ujenzi wa mtambo wa mafuta bandarini, alitakiwa kuviacha vifaa hivyo.
Mawaziri waliobaini kuondolewa kwa kipengele hicho kilichokuwepo ndani ya mkataba, ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda; Waziri wa Fedha na Uchumi, Wiliam Mgimwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Hayo yalibainika jana baada ya mawaziri hao kufanya ziara bandarini na kupata taarifa fupi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande.
Akizungumza na wafanyakazi wa bandari, Dk. Mwakyembe alisema wamefanya ziara hiyo ya kawaida ya kutembelea chombo hicho muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.
Alisema yeye na wenzake wamekubaliana kuwa wanahitaji maelezo haraka kuhusu watu hao waliondoa kipengele hicho kwenye mkataba, kwani hiyo ni hujuma na endapo mtambo huo utapata hitilafu watashindwa kufanya kazi.
Dk. Mwakyembe aliitaka bodi iitishe kikao cha dharura ili hadi leo lipatikane jibu kwani ana imani watu hao wanajulikana na hawapo mbali.
“Ni kitu cha kushangaza kuona mkataba uliokwishasainiwa unavunjwa kiujanja… kama mnavyofahamu mkataba ukishaafikiwa hakuna wa kuuvunja, sasa tunaomba hadi Jumatatu mtuletee jibu ili tulifanyie kazi kwa pamoja,” alifafanua Dk. Mwakyembe.
Alisema wanasheria wapo na kama inavyofahamika mkataba ukishapitishwa hauguswi tena, hivyo kama yupo aliyekichomoa kipengele hicho basi atambue kuwa na yeye atachomolewa.
Mbali na hilo, akizungumzia mashine ya utambuzi wa mizigo kwenye makontena (Scan), inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), Dk. Mwakyembe alisema hawaelewi kulikuwa na sababu gani za msingi mashine hiyo kupelekwa Tanga ambako ni zaidi ya miaka miwili sasa haifanyi kazi.
“Sasa kama haifanyi kazi imepelekwa kufanya nini au inacheza taarab?” alihoji Dk. Mwakyembe.
Aliiagiza TPA kuirudisha mashine hiyo ili ziweze kuwa mbili katika kuimarisha utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Vilevile amewataka wafanyakazi hao kujijengea tabia ya uadilifu kwani hiyo ni moja ya njia itakayosaidia kuwajengea imani wateja wao wa ndani na nje ya nchi.
Awali Mkurugezi wa TPA, Kipande, alisema nchi inayotegemea usafirishaji wa mizigo kwa kutumia barabara iko hatarini kufilisika.
Alisema TPA inaomba serikali kuimarisha ujenzi wa reli zinazoelekea kwenye bandari zake zote zikiwemo zile maziwa.