Wananchi waliliondoa gari lililoangukiwa na jengo la ghorofa 16 wiki iliyopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 35. Picha na Ibrahim Yamola
Dar es Salaam.
Kuporomoka jengo lililopo Mtaa wa Indira Gandhi Jijini Dar es Salaam, huenda ikawa mwanzo tu wa kuporomoka majengo mengine zaidi hasa kufuatia matokeo ya tume iliyoundwa mwaka 2006 iliyobaini zaidi ya majengo 100 Jijini Dar es Salaam yamejengwa bila kuzingatia viwango.
Kwanini Serikali haichukui hatua kwa majengo hayo 100 yaliyobainika kuwa hayajajengwa kwa kuzingatia viwango? Wenye akili timamu wanaweza kuendelea kujiuliza maswali mengi zaidi na kujibu wanavyoweza.
Wapo wanaoweza kusema rushwa ndio inasababisha mambo mengi kutofanyiwa kazi kwa ufasaha, lakini mbele ya sheria utaombwa utoe ushahidi, hapo bila shaka patafanya wengi kubadili maneno kwamba aaah labda Serikali inaendelea kufanya mchakato, mpango mkakati, mkakati yakinifu nk dhidi ya majengo hayo.
Kubomoa jengo lenye ghorofa 16 au hata chini au zaidi ya hapo baada ya kulibaini halijazingatia viwango, ni lazima uwe na uso mgumu. Baadhi ya wananchi wanasema wenye majengo bila shaka hawawezi kutulia wakisubiri sheria ifanye inachotakiwa kufanya, hapo ndipo ugumu unapoanzia.
Pinda analo na kujibu
Baadhi ya watu wanafikiri kuondolewa madarakani kwa viongozi walio katika wizara husika na sakata hili akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye ofisi yake ilichunguza na kubaini maghorofa zaidi 100 kuwa ni feki, kunaweza kuwa ni mojawapo ya mambo muhimu kwa sasa.
Mke na watoto wafukiwa
Licha kwamba jengo hilo liliporomoka saa 2.30 asubuhi, baadhi ya watu waliofukiwa na kifusi cha jengo hilo walikuwa wakiwasiliana na jamaa zao kwa njia ya simu na wengine wakipiga kelele za kuomba msaada.
Idd Baka ambaye alikuwa akiwasiliana na mkewe ambaye aliegesha gari huku ndani kukiwa na watoto wake wawili alikwenda dukani kununua bidhaa, mara jengo hilo likaporomoka, alikuwa akiwasiliana nae hadi majira ya mchana simu ya mke wake haikuwa inapatikana.
Vifaa duni
Ni dhahiri kwamba endapo kungekuwapo na vifaa vya kutosha katika zoezi la uokoaji lingewezaa kufanikiwa kwa muda mfupi na kwa kiasi kikubwa hivyo kuwapata majeruhi wakiwa hai.
Katapila latumika
Cha ajabu na aibu kwa taifa kutokuwa tayari kwa kuwa na vifaa vya kuokolea kwani tangu saa 2:30 hadi ilipofika saa 4.30 ndipo lilipatikana katapila moja ambalo nalo halikuwa na tija kutokana na kuwapo kwa uwezekano wa kuwakandamiza au kuwajeruhi zaidi watu waliofukiwa na kifusi hicho.
Kutokana na kutokuwepo na vifaa vya kukatia nongo waokoaji iliwachukua takribani dakika 15 kukata nondo zilizokuwa zimemkandamiza.
Umati wa watu ulivamia kifusi na kuanza kukisomba kwa mikono ili hali jambo hili lilikuwa kama mchezo wa kuigiza ambao umegharimu uhai wa watu zaidi ya 35 pamoja na kuharibu magari yaliyobondwa na kuwa kama chapati takribani matano.
Mashuhuda
Ali Mparang’ombe mmoja wa mafundi wa jengo hilo anasema kudondoka kwa jengo hilo ni mtiririko wa majengo mengine kutokuwa katika viwango vinavyotakiwa.