Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Peter Pinda
HALI ya usalama mkoani Mtwara bado tete baada ya jana Jeshi la Polisi kuwahamishia mkoani Lindi waandishi wa habari 150, waliokuwa katika mkutano wa siku tatu wa Kongamano la Nane la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uliofanyika Mtwara.
Waandishi hao walitoroshwa na polisi jana saa 11:00 alfajiri kwenda mkoani Lindi ambapo pia polisi walifanikiwa kusitisha maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), kwa lengo la kutaka kupata tathmini ya mwendelezo wa miradi ya gesi na maji.
Habari zinasema wananchi hao walitaka kuwateka waandishi wa habari kwa madai kuwa waliandika habari za kuzimwa kwa uasi wao kuhusu gesi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jambo wanalodai siyo kweli.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, alisema kuwa taarifa hizo zilikuwa ni tetesi tu, akiongeza kwamba katika Mkoa wa Lindi kulikuwa na taarifa kwamba yangefanyika maandamano makubwa, lakini hakuna kilichotokea.
“Ulikuwa ni uvumi wa watu, unajua hivi sasa anaweza kuibuka mtu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kuhusu jambo lolote tu, ila suala hilo la waandishi wa habari ni kweli na asubuhi niliambiwa na OCD, lakini hali ni shwari sasa,” alisema.
Mgogoro wa gesi uliibuka mwishoni mwa mwaka jana, baada ya Serikali kutangaza mpango wake wa kutandaza bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi wa mkoa huo walipinga mpango huo huku wakiungwa mkono na watu wa kada mbalimbali nchini, vikiwamo vyama vya siasa.
Katika kuonyesha kutotaka gesi itoke mkoani humo, wananchi hao walifanya maandamano, sambamba na kuchoma moto nyumba za baadhi ya wabunge, ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jengo la Mahakama ya Mwanzo Mtwara.
Januari 29 mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alizungumza na wananchi wa mkoa huo na kuwatuliza jazba, baada ya kueleza jinsi watakavyonufaika na gesi itakayozalishwa mkoani humo kabla ya kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es Salaam.
Pinda alisema kuwa hakuna tone la gesi ghafi itakayosafirishwa kwa njia ya bomba na kueleza kwamba kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajengwa katika Kijiji cha Madimba, mkoani humo na mabaki yatokanayo na gesi hiyo yatumike kuvutia uwekezaji wa viwanda.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Pinda ilipingwa na wananchi wengi ambao walidai kuwa imejaa siasa, ndiyo chanzo cha wananchi hao kutaka kuwateka waandishi wa habari kwa maelezo kuwa waliandika habari zenye kichwa cha habari ‘Pinda azima uasi Mtwara’, jambo ambalo walisema siyo kweli.
Madai ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara yalikuwa ni kupinga usafirishaji wa gesi ghafi kwenda Dar es Salaam, wakieleza kuwa mpango huo utafukuza uwekezaji wa viwanda mkoani humo, ambao ungechochewa na upatikanaji wa malighafi baada ya kusafishwa kwa gesi.
Pia walipinga ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi, Dar es Salaam wakiitaka Serikali kujenga mitambo hiyo mkoani Mtwara.
Mpango wa kutekwa waandishi
Taarifa za kuwapo uwezekano wa waandishi hao kutekwa zilifika kwenye vyombo vya usalama juzi usiku, kabla hazijafikishwa kwa waratibu wa ziara ya wanahabari hao, ambao walitekeleza mikakati ya kubadili muda wa kuondoka mkoani humo, ambapo badala ya saa 2:00 asubuhi walilazimika kuondoka saa 11:00 alfajiri.
Akizungumza mjini Mtwara, Augustino Joachim, mwendesha bajaji mjini humo, alisema kuwa katika siku za karibuni polisi mkoani humo wamekuwa hawavai sare na kutembea uraiani kama ilivyozoeleka, badala yake huzibeba kwenye mabegi na kuzivalia vituoni.
Alisema kuwa uhasama kati ya wananchi na askari polisi uliota mizizi tangu kutokea mauaji ya watu zaidi ya watatu, yaliyodaiwa kufanywa na polisi kwa kutumia risasi za moto.
Umiliki mabomu
Kutokana na kuwapo uhasama baina ya polisi na raia, inadaiwa kuwa wananchi mkoani humo wanamiliki mabomu ya kuvulia samaki ambayo watayatumia kukabiliana na askari polisi ili kuhakikisha gesi yao haiondoki.
Polisi Lindi wazuia maandamano
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Lindi jana limefanikiwa kusitisha maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), ambayo ilikuwa yafanyike jana katika Manispaa ya Lindi.
Kusitishwa kwa maandamano hayo kumetokana na barua ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Lindi, SP Yahya Mdogo ya Februari 20 mwezi huu, yenye kumbukumbu namba LIN/269/VOL101/320, ambayo iliandikwa kwa uongozi wa CUF, ikiwataka kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara.
Awali, CUF waliomba kufanya maandamano na mkutano wa hadhara Februari 8 mwaka huu, maombi ambayo yaliwasilishwa polisi na katibu wa chama hicho Wilaya ya Lindi, Abobakar Sahel.
Lengo la maandamano na mkutano huo ni kutaka kupata tathmini ya mwendelezo wa miradi ya gesi, maji, mfumo wa stakabadhi ghalani pamoja na kupata taarifa za kutekelezwa kwa ahadi zilizotolewa na Serikali juu ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata gesi na kutaka tafsiri ya mikataba ya gesi.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Lindi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lindi, Salum Baruani alisema kuwa maandamano hayo yamesitishwa kwa muda hadi Machi 3 mwaka huu.
“Tumepokea kwa masikitiko makubwa polisi kutumia nguvu kubwa kuzima maandamano haya na mkutano, kwani wametumia rasilimali nyingi kuleta askari kuzuia maandamano, rasilimali ambazo wangeweza kuzitumia katika mambo mengine ya maendeleo,” alisema Baruani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema kwamba polisi imezuia maandamano hayo, lakini CUF waliandika barua nyingine wakisisitiza kuwa wataandamana kwa nguvu.
“Tumeimarisha ulinzi ikiwa ni pamoja na kupekua magari yote yanayoingia na kutoka mkoani Lindi, ili kuhakikisha abiria wanaoingia ni salama,” alisema Mwakajinga.
Imeandaliwa na Tausi Mbowe, Mtwara, Mwanja Ibadi, Lindi na Fidelis Butahe, Dar