NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amesema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni mzigo katika serikali.
Amesema kuwa hii ni kutokana na kushindwa kufanya uamuzi mgumu katika masuala yanayolihusu taifa licha ya baadhi ya mambo kuwa katika mamlaka yake.
Zitto alisema kuwa hivi karibuni Pinda alishindwa kusimamia muswada wa sheria ya marekebisho ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, hali iliyosababisha kutokea vurugu bungeni.
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika kata ya Inyonga na Songambele wilayani Mlele, mkoa wa Katavi, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya kuimarisha chama Kanda ya Magharibi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona Waziri Mkuu akishindwa kukutana na kiongozi wa upinzani bungeni na kujadili masuala muhimu ya kitaifa kabla ya Bunge kuanza kwa ajili ya mustakabali wa taifa.
Akitolea mfano masuala kadhaa ambayo Pinda ameshindwa kuyasimamia na kumsubiri Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuyafanyia uamuzi, Zitto alitaja sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, na Yule wa Wizara ya Afya na sasa suala la kuhakikisha muafaka unapatikana katika suala muhimu la Kikatiba.
“Kama tunaye Waziri Mkuu anayekaa bungeni na kushika tama wakati nchi ikiwa katika hali ngumu ni tatizo. Huyu kila jambo anasubiri Rais atoke UN kuja kufanya uamuzi ambao yeye angeweza kuusimamia. Basi tuna kazi ya ziada katika kupata maendeleo,” alisema.
Zitto alifafanua kuwa mwanzoni alidhani Pinda anashindwa kusimamia majukumu ya serikali kutokana na kukabiliwa na jitihada za kuboresha miundombinu na maisha ya wakazi wa jimbo lake hali aliyoelezea kuwa ni tofauti na aliyoikuta.
Alisema kutokana na hali hiyo ya Pinda kutokuwa na mamlaka, wakulima wa Katavi wameendelea kununua mbolea kwa gharama ya juu licha ya serikali kutenga kiasi cha bilioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya ruzuku ya mbolea kote nchini.
Alisema fedha hizo zinaliwa na wajanja huku serikali ikiendelea kuwa katika hali ya usingizi wa pono.
Tofauti ya CCM, CHADEMA Akizungumzia sababu ya ziara yake katika kanda hiyo, Zitto alisema ni kwa ajili ya kuhimiza mbegu ya ukombozi wa fikra na maendeleo kutoka katika mikono ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alisema wakati CHADEMA inapambana katika kila kona kuhakikisha udhalimu unaofanywa na serikali unaondoka, CCM inatumia kila njia kuhakikisha inawanyonya wananchi.
“Tofauti kubwa kati ya vyama hivi ni kwamba CCM inaishi kwa kuwanyonya wananchi na CHADEMA imesimama kidete kutaka udhalimu huo uondoke; na kwa ajili hiyo chama hicho tawala kinatumia kila propaganda kuhakikisha wananchi hawatuungi mkono,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, kazi ya CHADEMA siku zote imekuwa ni kuwafumbua macho wananchi juu ya unyonyaji unaofanywa na serikali ya CCM na kuwataka waepukane na propaganda za kwamba kuiunga mkono CHADEMA ni kukaribisha vita nchini.
Alisisitiza kuwa kwa sasa CHADEMA inajiandaa kushika dola mwaka 2015 na kwamba wanasimamia upatikanaji wa Katiba bora itakayowafanya wanasiasa kuwa watumishi wa wananachi badala ya kuwa watawala.
“Mmetuona kwa uchache wetu bungeni tumeweza kufanya mambo makubwa kwa nchi kila kashfa ya ufisadi mnayoisikia leo ni wabunge wa upinzani wameibua na si wa chama tawala,” alisema.
-Tanzania daima
No comments:
Post a Comment
gfjythfghgfhdfgergdfgbvdfgrfdgdfrgdrgdfrgrdegedrgdrfg