Hatua ya Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania, Augustino Ramadhani
kujitosa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais
imewavuruga wagombea wenzake wa urais na kuibua mjadala mzito katika
maeneo mbalimbali nchini.
Mitandao ya kijamii ilijaa mijadala
inayohusu kuingia kwake katika kinyang’anyiro hicho, huku baadhi ya
wapambe wa wagombea wakieleza wazi kukatishwa tamaa na mgombea huyo
ambaye wasifu wake unaonyesha ana sifa za ziada zaidi ya baadhi ya
wagombea.
Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa ni sifa
ambazo CCM huzitumia bila kuzitaja, hasa kile kinachoitwa zamu kati ya
Bara na Zanzibar na nyinginezo, ikielezwa kuwa akihitajika mgombea
kutoka Zanzibar kumrithi Rais Jakaya Kikwete, Jaji Ramadhani anaonekana
kufaa zaidi.
Katika mijadala hiyo, wapo waliohusisha
hukumu alizowahi kuzitoa akiwa Jaji na baadaye Jaji Mkuu kwamba
zililenga kukibeba chama hicho tawala kwa sababu anaonekana alikuwa na
mapenzi nacho siku nyingi lakini wengine walieleza kuwa hawaoni tatizo
kwa jaji huyo ambaye ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.
Wakati maoni ya wananchi yakitofautiana
juu ya hatua ya Brigedia Jenerali huyo mstaafu kuchukua fomu, mwenyewe
aliliambia gazeti hili jana kwamba kwa sasa si jaji tena, hivyo ana haki
ya kugombea urais na hakuna kanuni wala sheria inayomzuia.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa
swali kuhusu Ibara ya 113A ya Katiba ya Tanzania inayotajwa kumzuia,
ikisema; “Itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa
Mahakama Kuu, Hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote cha
siasa, isipokuwa tu kwamba atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa
katika ibara ya 5 ya Katiba.”
“Ukisoma
Ibara hiyo inasema kama mhusika ni jaji. Mimi huko nimeshaondoka sasa
nitashindwa kugombea kwa lipi? Wacha watu waibue mambo tu, lakini hata
ukisoma Katiba utaona mwenyewe wao wanazungumzia past tense (wakati
uliopita), sasa tunazungumzia present tense (wakati uliopo),” .
Kuhusu mapenzi kwa CCM yanayoweza kuathiri utendaji, Jaji Ramadhani alihoji, “Hukumu gani niliipendelea? Hakuna kitu kama hicho.
Kuanzia 1961 tulivyopata uhuru, majaji
hawakuwa kwenye chama? Sasa kuna ajabu gani mimi kuwa katika chama maana
kipindi hicho kulikuwa na chama kimoja tu, watu wote walikuwa katika
chama si majaji tu.
“Zamani (wakati wa chama kimoja),
ulikuwa huwezi kupata kazi ya aina yoyote kama wewe si mwanachama. Leo
ajabu ni mimi tu. Hata wanahabari ilikuwa lazima wawe wanachama.”
Jaji Ramadhani ambaye alikuwa Makamu
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, juzi mchana
alichukua fomu kuwania nafasi hiyo ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano
huku akisema; chema chajiuza, kibaya chajitembeza.
Katika maelezo yake alisema alikuwa
mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu tangu Agosti, 1969 wakati huo
akiwa mwanafunzi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
MWANANCHI
Siku moja baada ya kuhukumiwa kulipa
faini Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la shambulio la
kawaida dhidi ya aliyekuwa mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu
uliopita, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kuwania tena ubunge katika jimbo hilo.
Mbowe aliyeepuka kwenda jela kwa kulipa
faini hiyo juzi, alitangaza uamuzi huo jana alipokuwa akihutubia mkutano
wa hadhara katika eneo la stendi ya zamani mji mdogo wa Bomang’ombe,
Kilimanjaro.
Mwenyekiti huyo alifikia hatua hiyo
baada ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo kumshinikiza agombee
ubunge na kumchangia Sh800,000 za kuchukua fomu ambayo ndani ya Chadema
hugharimu Sh250,000.
“Nashukuru
kwa walioanzisha wazo hili lakini zaidi ninawashukuru waliojitolea
kunichangia fedha. Nimekubali nitagombea ubunge katika uchaguzi ujao,” alitangaza Mbowe na kufanya uwanja kulipuka kwa shangwe.
Mbowe aliyeambata na wabunge kadhaa
akiwamo Philemon Ndesamburo wa Moshi Mjini, alijinasibu kuibuka na
ushindi wa kishindo yeye na chama chake katika uchaguzi ujao kuanzia
jimbo la Hai na katika majimbo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kama sheria ingekuwa inaruhusu
ningefurahi iwapo CCM ingesimamisha wagombea zaidi ya 10 katika Jimbo la
Hai ili wapambane na mimi kwa sababu mgombea mmoja pekee siyo saizi
yangu,” alijinasibu Mbowe.
Hukumu dhidi yake
Akizungumzia hukumu iliyomtia hatiani na
kuhukumiwa faini au kifungo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani
Bungeni alisema alikusudia kwenda jela kuwakilisha mamilioni ya
Watanzania wanaosota huko “kwa kesi na hukumu za kipuuzi”.
“Kama kesi ya mtu mwenye dhamana ya
uwakilishi wa wananchi kwa nafasi ya ubunge inaweza kuendeshwa kwa zaidi
ya miaka minne na hukumu kutolewa katika mazingira tatanishi kama
ilivyokuwa kwangu, Watanzania wa kawaida wanateseka kiasi gani?” alihoji
Mbowe.
Alidai kuwa baada ya kumhukumu kifungo
cha mwaka mmoja au faini ya Sh1,000,000, Hakimu Denis Mpelembwa
amepandishwa cheo kuwa hakimu mkazi na kuhamishiwa mkoani Kagera, siku
moja tu baada ya hukumu.
“Kilichokuwa
kinatafutwa ni namna ya kumzuia Mbowe asigombee ubunge Hai kwa sababu
CCM wanajua nguvu yangu. Wamekosea sana kwa sababu hukumu ile hainizuii
kugombea. Nitaombea na nitashinda kwa kishindo,” alisema.
HABARILEO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
amesema hivi sasa nchi haihitaji Rais asiyetambulika nchi za nje kwani
atapoteza muda mwingi kujitambulisha badala ya kushughulikia masuala
mbalimbali ya wananchi wake.
Membe alitoa kauli hiyo mjni hapa jana
wakati akizungumza na wanachama wa CCM waliomdhamini kwenye safari yake
ya uhakika pamoja na wananchi waliokuja kumsikiliza.
“Tunataka
Rais anayejulikana ndani na nje ya nchi si Rais ambaye atalazimika
kupiga hodi kila nchi kujitambulisha kwani hatma ya Watanzania milioni
48 iko mikononi mwake,” alisema Waziri Membe na kuongeza;
“…Mtu
kabla ya kuomba nafasi hiyo ya juu ya uongozi anahitaji kujiridhisha
kwanza ndipo aweze kufanya uamuzi sahihi wa kuomba nafasi hiyo, mimi
nimejipima nimejiona ninatosha kuwaongoza Watanzania katika masuala ya
utawala bora.”
Alisema kuwa cheo cha urais hakijaribiwi
kwani ni nafasi ya juu sana ambayo anayechaguliwa anapaswa kuangalia
hatma ya nchi na watu wake.
Akiwa mkoani Singida, Waziri Membe
alifanikiwa kupata wadhamini 1,905 idadi ambayo alisema si haba na
kuwashukuru wananchi kwa moyo wa imani walioonesha kwake.
HABARILEO
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda amesikitishwa na wimbi la wabunge kutofika kwenye vikao vya mjadala wa bajeti ya serikali mwaka 2015/16.
Kwa kiasi kikubwa, hali hiyo inaelezwa
inatokana na homa ya ubunge, wengi wakionekana kuelekeza akili zao
katika majimbo yao ili kujiweka sawa na hatimaye warudi madarakani baada
ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Makinda ambaye aliongoza kikao cha juzi,
ikiwa ni mwendelezo wa mjadala wa siku saba wa kuchangia mjadala wa
bajeti, alijikuta akikosa maneno ya kuzungumza kutokana uchache wa
wabunge wakati wa kuanza kikao cha jioni.
“Haya tuanze kuzungumza wenyewe sasa,” alisema
Makinda kabla ya kumtaka Katibu wa kamati kusoma ratiba za shughuli za
bunge kwa jioni hiyo ambapo wabunge waliokuwamo katika ukumbi wa bunge
hawakuzidi 20.
Bunge lina zaidi ya wabunge 300.
Alipokuwa akiahirisha bunge kwa siku ya juzi, Spika alisema: “Ninyi
(wabunge) mnaobaki huko na kufuatilia majadala kwa kuangalia kwenye
televisheni, sio vizuri.
Ni vyema kuwapo kwenye mjadala wa hii
bajeti na kwa hili mtajifunza mambo mengi.” Wiki iliyopita alipokuwa
akielezea mjadala wa bajeti kuwa utajadiliwa kwa siku saba, aliwaonya
wabunge kutokuwa watoro katika vikao vya majadiano ya pamoja na kufahamu
kuwa wabunge wengi wanajoto la uchaguzi.
Aidha, akichangia mjadala juzi jioni,
Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomar Khamis (CCM) aliitaka Serikali
kuhakikisha inawachukulia hatua za kinidhamu ikiwa na kuwafukuza kazi
watendaji ambao watakwamisha juhudi za kukusanya kodi.
“Hakuna
haja ya kumhamisha mtendaji wa serikali ambaye atashindwa kukusanya
kodi, maana kwenye utumishi kuna wafuasi wa CUF, CCM hata Chadema ambao
wanaweza kuhujumu juhudi za serikali,” alisema.
Kuhusu tozo ya mafuta alitaka mafuta ya
taa pia yapandishwe kwa Sh 50 kwa lita tofauti na mapendekezo ya
serikali ya Sh 150 jambo ambalo litawaumiza wananchi wengi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha
(Chadema), aliitaka serikali kuhakikisha wanajizatiti katika kubana
mianya ya biashara za magendo na bandari bubu, ili kuiwezesha TRA
kukusanya mapato ya uhakika kwani kumekuwa na wimbi kubwa la watanzania
kufanya biashara za magendo na kupitisha bidhaa kwenye bandari bubu
linalokosesha serikali mapato.
JAMBOLEO
Penina Joseph mkazi wa kijiji cha Mrito Mkoani Mara amegeuka bubu baada ya kung’atwa na mamba.
Baba wa mtoto huyo Joseph Mngule alisema
binti yake alishambuliwa na mamba Oktoba mwaka jana na hadi sasa hawezi
kuzungumzo lolote.
Mungule alisema kabla binti yake
hajashambuliwa alikua akizungumza kama kawaida huku akiendelea na masomo
yake ya msingi lakini ba ada ya tukio aligeuka kuwa bubu na hivyo
kushindwa kuendelea na masomo.
“Ukimwambia
kitu anasikia na kutekeleza lakini hawezi kuzungumza, tuliambiwa na
daktari huenda baadhi ya mishipa imekata mawasialino”Joseph.
Baba huyo alisema tangu kuugua kwa mtoto
wake, tayari ametumia zaidi ya milioni 12 baada ya kuuza mali zake ili
kuokoa maisha ya mtoto wake.
Pia alisema hilo sio tukio la kwanza kwa
kijiji hicho kwani tayari watu sita wameuawa na mamba na wengine 30
kujeruhiwa huku ng’ombe, mbuzi na mbwa nao wakishambuliwa kwa wingi.
NIPASHE
Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa amezidi kupata ma elfu ya wadhamini huku akisema kutokana na wingi wa watu kujitokeza tayari ameshafunga magoli ya Urais.
Lowassa aliwasili jana katika Mkoa wa Kilimanjaro akitokea Tanga na kupata wadhamini 33,780 katika Mkoa huo.
Lowassa alisema anajivunia rekodi yake kwa Watanzania kutokana na kumjua na kujua nguvu yake katika utendaji kazi.
“Nadhani wale wenzangu 36 wakiona umati
huu watajua na kujionea kuwa nimeshafunga magoli, tena magoli yenyewe ni
sawa na yanayofungwa na kina Ronaldo na Messi hayana ubishi”Lowassa.
Alisema nia yake ya kugombea Urais ni
kutokana na kujiamini, ana uwezo, anatosha na amegomea ili ateuliwe na
chama hicho aweze kupambana na umaskini katika Taifa lenye rasilimali
nyingi.
NIPASHE
Waandishi wa habari jana walizuiwa kuripoti kesi ya ugaidi
inayowakabili viongozi 23 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu
Zanzibar (JUMIKA), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa 3:15 asubuhi na
kupelekwa kwenye chumba cha mahakama ya wazi namba moja wakiwa chini ya
ulinzi mkali wa askari polisi na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU), waliokuwa wamebeba silaha na mabomu ya machozi.
Baada ya kuingia mahakamani hapo wakiwa wanamsubiri hakimu
anayeisikiliza kesi yao, waandishi wa habari walijisogeza kutaka kuingia
kwa lengo la kuripoti kesi.
Lakini cha ajabu, walipofika askari wa FFU waliokuwa wamebeba silaha
na askari kanzu wa magereza waliokuwa wameuzingira ukumbi huo,
waliwakataza waandishi kusogelea mlango wa kuingilia.
Hata hivyo, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Jackson Chidunda
alidai kuwa upande wa mashtaka wameiomba mahakama na imeridhia kuwa
kuanzia jana, waandishi wa habari hawapaswi kuripoti tena kesi hiyo kwa
sababu za kiusalama na kiintelejensia.
Chidunda alidai kuwa ombi hilo lilitolewa mahakamani hapo na Wakili
wa Serikali, Peter Njike mbele ya Hakimu Mkazi, Renatus Rutta kupitia
kifungu cha 34 (4) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Kwa upande wa mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Ubaidu Hamidu na Abdulfattah Abdallah
walidai kuwa upande wa mashtaka waliomba waandishi wa habari kuzuiwa
kuripoti kesi hiyo kwa sababu inasadikiwa kuna watu wanarekodi na kwenda
kurusha mwenendo wake katika mitandao ya kijamii, kitu ambacho ni
kinyume na matakwa ya Mahakama.
No comments:
Post a Comment
gfjythfghgfhdfgergdfgbvdfgrfdgdfrgdrgdfrgrdegedrgdrfg