Ebola: Ugonjwa hatari unaoitesa jamii Afrika | Send to a friend |
Friday, 17 August 2012 09:37 |
Na Florence Majani KATIKA siku za hivi karibuni ugonjwa wa Ukimwi umetajwa kuwa si janga tena hasa baada ya mwanga wa tiba yake kuanza kuonekana- njia za kuzuia na dawa za kufubaza makali ya virusi vyake kupatikana. Lakini, Afrika inaendelea kusumbuliwa na maradhi mengi mno, kiasi cha kutatiza afya za wakazi wake. Miongoni mwa magonjwa hayo ni malaria, ambao unasemekana kuua watu wengi zaidi barani humo. Lakini, ugonjwa wa ebola ambao umeikumba nchi jirani ya Uganda hivi karibuni baada ya miaka ya karibuni kutesa wengi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), unatajwa kuwa ni ugonjwa hatari zaidi pengine kuliko Ukimwi kwa namna unavyomtesa mgonjwa, unavyoua kwa haraka na unavyoambukiza kwa wepesi. Mwananchi lilifunga safari na kuzungumza na daktari Henry Mwakyoma, Mkuu wa Kitengo cha Patholojia wa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili (MNH). Dk Mwakyoma anaulezea ugonjwa huu kama ugonjwa wa hatari zaidi ambao wanasayansi wameshindwa kupata tiba yake hadi sasa. Daktari huyu anasema ebola ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya ‘ebola’ ambavyo hupatikana kwa wanyama wa porini hasa waishio katika maeneo yenye joto katika nchi za Afrika. Jina la ugonjwa huo, yaani ebola, limetokana na Mto Ebola, uliopo nchini DR Congo. Dk Mwakyoma anaongeza kuwa zipo aina tano za virusi vya ugonjwa huu na majina yake yamepatikana kulingana na mazingira yake. Kwa mfano kirusi cha ebola cha nchini Uganda kinaitwa ‘Bundibugyo Virus’ na kile cha DRC kimepewa jina la ebola. Kirusi cha nchini Sudan kimepewa jina la Sudan Virus na nchini Ivory Coast kimepewa jina la Tail Virus. Anaongeza: “Aina ya tano ya kirusi cha ebola ilipatikana Amerika ya Kusini, lakini kirusi hiki hakijabainika kusababisha madhara kwa binadamu.” Ebola yaingia duniani Tukio la kwanza la ugonjwa hatari wa ebola liligundulika Agosti 29, 1976 katika eneo la nyanda za juu nchini DR Congo, liitwalo, hususan Yambuku. “Ugonjwa huu uliwapata wakazi wa Yambuku ambao inasemekana walikuwa wakila mizoga ya wanyama wa porini, hasa sokwe na popo,” anasema mtaalam huyo. Mwaka huo huo ugonjwa huo uliibuka nchini Sudan katika maeneo ya viwanda vya pamba, katika mji wa Nzara na mwaka 1994, ugonjwa huu uliibuka nchini Ivory Coast na kusababisha maafa makubwa. ‘Ugonjwa wa ebola uliibuka nchini uganda Julai 2007 katika wilaya ya Bundibugyo,” anasema Dk Mwakyoma. Binadamu hupataje ebola? Dk Mwakyoma anasema utafiti uliofanyika miaka ya nyuma uliabini kuwa virusi vya ebola huingia kwa mwanadamu kutoka kwa wanyama wa porini, hasa sokwe na popo. “Baada ya binadamu kula nyama yenye virusi hivyo, husambaa na katika mwili wake, na huo ndiyo mwanzo wa wanadamu wengine kupata maradhi hayo,” anasema. Anaongeza kuwa utafiti huo uligundua kuwa baadhi ya wanyama wanaweza kuishi na virusi vya Ebola bila kuwadhuru na wanyama wengine huweza kudhurika na kufa kama wanavyoathiriwa wanadamu. Binadamu hawezi kuambukizwa Ebola kwa njia ya upumuaji, bali hupata kwa njia ya majimaji ya mwilini mwa mwanadamu. Majimaji hayo ni pamoja na damu, jasho, kamasi, kinyesi na wakati mwingine mbegu za kiume pamoja na vifaa ambavyo mgonjwa anayeugua ebola atakuwa amevitumia. “Ndiyo maana tunasema ugonjwa huu ni hatari zaidi kwa sababu, ni kwa sekunde chache tu ukifanya mchezo umeambukiwa na kifo chake ni cha haraka sana,” anasema. Dk Mwakyoma anasema virusi vya ebola hupendelea kukimbilia katika mishipa ya damu na hivyo huenda kuathiri ogani muhimu mwilini ambazo huufanya mwili ujiendeshe. Ogani ambazo huathiriwa zaidi ni ini, figo, mishipa midogomidogo ya damu, mfumo wa chakula na mfumo wa upumuaji. Dalili za ugonjwa huu Dalili za awali za ugonjwa huu, Dk Mwakyoma anaeleza kuwa huanza kuonekana kuanzia siku ya kumi hadi wiki mbili baada ya binadamu kupata maambukizi. Anazitaja dalili za mwanzo kuwa ni mafua makali ambayo si mafua ya kawaida kama ambayo wengi wetu huugua, la hasha, bali ni mafua ya kipekee. Lakini pia, mtu aliyepata uambukizo wa virusi vya ebola huchoka mwili, hupata homa inayoambatana na vipele vidogovidogo kama vile vya kusisimkwa. “Mgonjwa hupata maumivu makali katika viungio vya mwili (joints),misuli na maumivu ya kifua. Lakini, pia kadri siku zinavyosonga mbele, mgonjwa huendelea kupata madhara mengine,” anasema Madhara hayo ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa chakula jambo linalosababisha mgonjwa kutapika , kukosa hamu ya chakula na wakati mwingine kuharisha. Virusi hivyo huendelea na kwenda mpaka katika mfumo wa njia ya hewa, virusi hivyo vinaposhambulia mfumo huo mgonjwa huanza kukohoa, kupata kwikwi kwa kiwango cha juu na kuwashwa koo. “Virusi hivi ni vya hatari zaidi kwani humfanya mgonjwa akaathirika hata katika mfumo wa neva za fahamu kwani baadhi huanza kuchanganyikiwa akili, kichwa kuuma sana, kuchoka na kupata degedege(seizures) na mwisho mgonjwa huwa mahututi (coma),” anaeleza Dk Mwakyoma Vilevile, mgonjwa wa ebola huathirika katika ngozi kwani hutokewa na vibaka vidogo sana vyenye ukubwa wa tundu la sindano, vilivyovilia damu. “Vitundu hivyo vya damu hutokana na kuathiriwa kwa mishipa ya damu mwilini na kwa kitaalamu huitwa ‘maculo paular rashes. Vitundu hivyo huonekana chini ya ngozi ya mgonjwa,” anasema. Anasema baada ya muda vitundu hivyo huwa vikubwa na huanza kuvuja damu endapo mgonjwa atachomwa na kitu chenye ncha kali kama sindano na damu huendelea kutoka kwa wingi kadri siku zinavyokwenda. “Dalili ya mgonjwa kutokwa damu ni mbaya na mara nyingi hupelekea kifo, kwa sababu damu hiyo haitoki nje peke yake, bali hutoka ndani kwa ndani mwilini mwa mgonjwa” anasema. Dk Mwakyoma anasema: “ Kifo kwa mgonjwa wa ebola husababishwa na mchanganyiko wa mambo mengi. Kwanza ni kushuka kwa mapigo ya moyo(hypertension), kufa kwa ogani za mwilini kama ini, figo, ubongo na kupoteza damu na maji mengi,” Anasema ndiyo maana mgonjwa wa ebola huteseka na hufa baada ya muda mfupi kwa sababu mwili wake hushambuliwa kwa kiasi kikubwa kwa muda mfupi. “Kingine kibaya zaidi ni kupoteza damu, kwani mgonjwa anaweza kuwa anatapika damu, anaharisha damu nyeusi, na anakohoa damu,” anasema Tiba Mtaalam huyo anasema hadi sasa hakuna tiba ya ugonjwa wa ebola. Anasema asilimia 70 ya watu wanaougua ugonjwa huu hufa. Anaongeza kuwa hiyo ni sababu kubwa inayoufanya ugonjwa huu uwe hatari zaidi kwani mgonjwa awahi au asiwahi matibabu, kama ameupata ugonjwa huu, hawezi kupona. “hakuna tiba ya ugonjwa huu, bali mgonjwa hutibiwa dalili au magonjwa yanayomkumba, kwa mfano, akiishiwa damu huongezewa damu, akiishiwa maji, huwekewa maji au kumshusha homa iliyopanda,kukohoa au kutapika” anasema Lakini, anasema kwa kuwa ebola huambukizwa kwa wepesi usio wa kawaida, mgonjwa hutengwa kabisa na jamii na wanaomshughulikia kwa mfano madaktari, hutakiwa kuvaa kinga za hali ya juu. Dk Mwakyoma anaeleza kuwa asilimia 30 ya watu wanaopona ugonjwa wa ebola huweza kubaki na virusi hivyo na kuendelea kuambukiza kama VVU vinavyobaki kwa watu wanaotumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs). Anasema wengi wanaopona hubaki na madhara kama nywele kunyonyoka, macho kuathiriwa kwa kutokwa machozi, au kudhuriwa na mwanga, na kwa wengine virusi vya ebola hubaki katika mbegu za kiume na kike. “Virusi vya ebola ambavyo vinatajwa kubaki katika mwili wa mwanadamu na kuendelea kudhuru wengine ni virusi vya Sudan. Kwa mfano, mwanaume ambaye aliugua ebola akapona, huweza kumwambukiza mke wake kwa njia ya kujamiiana na kusababisha ugonjwa huo kulipuka kwa mwanamke,” anafafanua Dk Mwakyoma anasema ugonjwa wa ebola ni wa hatari zaidi na kuwa ni vyema kama maeneo ya mipakani yakaongezewa ulinzi lakini pia alishauri watu kuacha kula baadhi ya wanyama wa porini wanaotajwa kuwa na virusi hivyo. |
No comments:
Post a Comment
gfjythfghgfhdfgergdfgbvdfgrfdgdfrgdrgdfrgrdegedrgdrfg